HADUBINI YAPITWA NA PANYABUKU KWA UTAMBUZI WA VIMELEA VYA KIFUA KIKUU

Katika kuboresha huduma ya kubaini vimelea vya kifua kikuu na afya ya jamii kwa ujumla, Kituo cha Kudhibiti Viumbe Hai Waharibifu kikishirikiana na asasi ya kibelgiji ijulikanayo kama APOPO, wameweza kugundua ufanisi mkubwa wa panyabuku katika kubaini vimelea vya kifua kikuu ikilinganishwa na hadubini.

Mkurugenzi wa Kituo cha Kudhibiti Viumbe Hai Waharibifu, Dr. Ladslaus Mnyone amethibitisha kuwa panyabuku wameonesha uwezo mkubwa wa kubaini vimelea vya kifua kikuu ndani ya muda mfupi ukilinganishwa na hadubini ambayo huhitaji rasilimali nyingi ikiwemo watu, muda, fedha na rasilimali nyinginezo.

Ndani ya dakika 20 panyabuku ana uwezo wa kubaini sampuli 120 hadi 150 za makohozi ambapo kwa njia nyingine kwa mfano hadubini inaweza kuchukua siku nne au zaidi kutambua sampuli hizo”. Aliongezea kwa kusema kuwa kituo kupitia teknolojia hiyo kimeweza kupanua wigo kwa kufanya kazi na nchi mbalimbali ndani na nje ya bara la Afrika, zikiwemo Ethiopia, Zimbabwe, Angola, Msumbiji, Israeli na Kolombia. Ndani ya Tanzania, zaidi ya kliniki 70 za kifua kikuu zinafaidika na huduma ya panya hao katika kufanya tambuzi za vimelea sababishi vya kifua kifuu (TB).

Kituo cha Kudhbiti Viumbe Hai Waharibifu kimelenga kupunguza gharama za kubaini vimelea vya kifua kikuu, kuongeza uwezo wa kubaini maambukizi ya kifua kikuu kwa wakati na kuharakisha upatikanaji wa tiba kwa wakati. Hii itapunguza kasi ya maambukizi ya kifua kikuu kwa sababu mlengwa anapoapata dawa kwa wakati na kupelekea vimelea vinapoteza uwezo wa kusambaa.

 

Related Posts